Tuesday, August 26, 2025

JINSI WALIMU WANAVYOISHI NA WANAFUNZI  WASUMBUFU

“MAISHA YA WANAFUNZI  SHULE” ni kitabu kinachoelezea maisha halisi ya wanafunzi shuleni na jinsi wanavyojenga au kubomoa maisha yao ya baadae  kulingana na tabia zao. 

Ni mwongozo bora kwa walimu, wazazi, walezi na wanafunzi wote wanaotaka kujua namna ya kukabiliana na changamoto za kimaadili, nidhamu ili kufikia mafanikio ya kitaaluma na maisha yanayokubalika kijamii inayowazunguka

SURA YA 1: MAISHA YA SHULE.

1.1: Maisha ya Shule ni Nini?

Maisha ya shule ni kipindi muhimu katika ukuaji wa mtoto, kinachojumuisha si tu kujifunza masomo ya darasani bali pia mafunzo ya kijamii, kiakili, kihisia na kitabia. Mtoto anapoingia shule kwa mara ya kwanza, anaanza safari ya kujifunza siyo tu kusoma na kuandika bali pia kujua jinsi ya kuwasiliana, kuheshimu wengine, na kushughulikia hisia zake. Kwa mtoto wa kabila kama Wazaramo ambaye analelewa katika familia ya pamoja, maisha ya shule yanaweza kumshangaza kwa sababu anaanza kujifunza kuwa sehemu ya jamii kubwa isiyokuwa ya familia tu. Umri wa kati ya miaka 6 hadi 13 ni muhimu sana kwa sababu ni kipindi cha ujifunzaji kwa kuiga, ambapo mtoto anaiga tabia za walimu, wazazi na wanafunzi wenzake. “Sikumoja rafiki yangu, Dastani alinisimulia kuwa wanafunzi wake walimuzli kitu na mazungumzo yalikuwa kamahivi”

Mwanafunzi A: "Mwalimu, kwanini tunapaswa kuvaa sare kila siku?"

Mwalimu: "Sare ni njia ya kuonesha usawa. Shuleni, hakuna tajiri wala maskini, nyote ni sawa."

Mwanafunzi B: "Lakini baba yangu alisema kabila letu halivalishwi sare."

Mwalimu: "Sawa, lakini hapa shule ni mahali pa kushirikiana tamaduni. Tunajifunza kuishi pamoja, hata kama nyumbani kuna tofauti."

Hii ni kwasababu watoto wanatoka mazingira tofauti, tabia zao huathiriwa sana na malezi yao ya nyumbani. Mtoto anayeishi mtaani na mzazi mlevi anaweza kuingia shule akiwa na tabia ya fujo au ukimya mkubwa. Hii si kwa sababu ana roho mbaya, bali ni matokeo ya mazingira aliyokulia. Saikolojia inaeleza kuwa mazingira ya mtoto katika miaka ya awali yanaunda sehemu kubwa ya tabia zake za baadaye.


1.2: Umuhimu wa Shule katika Malezi ya Mwanafunzi.

Shule ni sehemu ya pili ya malezi baada ya familia. Ingawa mzazi hutoa msingi wa kwanza wa maadili na nidhamu, shule huendeleza msingi huo kwa kumuweka mtoto kwenye mfumo rasmi wa kijamii. Hapa ndipo mtoto huanza kupata picha ya dunia halisi  kuna sheria, ratiba, kazi za pamoja na adhabu kwa makosa. Hii humsaidia mtoto kujifunza uwajibikaji, uvumilivu na kujipanga. Kwa mtoto wa kabila la Wamasai, ambaye anaishi kwenye jamii ya wafugaji, shule humtambulisha katika mfumo wa mpangilio wa muda na kanuni tofauti na maisha ya kawaida ya jamii yake.

“ Mzazi na mwanlimu wakizungumzia  utlivu wa mtoto ”


Mzazi: "Mwalimu, mtoto wangu siyo mchangamfu kama wengine. Anapenda kuwa kimya tu."

Mwalimu: "Ni kawaida kwa watoto waliokulia kwenye jamii tulivu au zisizo na misukumo mingi ya kijamii. Tutamshirikisha katika michezo polepole hadi ajifunze kushirikiana."

Mzazi: "Hivyo inasaidia kweli?"

Mwalimu: "Ndiyo. Kitaalamu, michezo ni tiba ya kihisia kwa watoto wenye msongo au woga."

Mtoto anaposhirikishwa katika shughuli mbalimbali za shule, anajifunza jinsi ya kujitambua. Hii huongeza hali ya kujiamini na kufungua njia ya kujifunza mambo mapya. Shule huimarisha uwezo wa kijamii ambao familia pekee isingeweza kutoa. Kwa mujibu wa mtaalamu wa saikolojia Erik Erikson, hatua hii ya maendeleo ya kijamii kwa mtoto ni sehemu muhimu ya kujenga utambulisho wake.

1.3: Uhusiano kati ya Mwanafunzi, Mwalimu na Wazazi.

Maendeleo ya mwanafunzi yanategemea sana jinsi walimu, wazazi, na mwanafunzi mwenyewe wanavyoshirikiana. Pale ambapo mwalimu na mzazi wanakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara, mtoto hujenga nidhamu, kujituma na kuwajibika. Pale ambapo kuna mgongano kati ya mzazi na mwalimu, mtoto hupata mchanganyiko wa maadili. Kwa mfano, mzazi anapomlinda mtoto wake hata anapokosea, mtoto anajifunza kuwa hakuna athari ya makosa, hivyo hushindwa kujifunza kuwa na wajibu. Katika baadhi ya makabila kama Wachaga, ambapo nidhamu na mafanikio ya elimu vinapewa kipaumbele, wazazi hujenga mawasiliano ya karibu na walimu  hali inayochangia mafanikio ya watoto wao.

“Mazungumzo  kati ya mzazi na mwalimu kuhusu uwajibikaji wa mwanafunzi katika kazi za darasani”:

Mwalimu: "Baba Yona, mtoto wako Yona huwa hajaleti kazi za nyumbani."

Mzazi: "Sawa mwalimu, nitazungumza naye. Labda hatuelewi uzito wa kazi hizo."

Mwalimu: "Tukishirikiana, Yona anaweza kubadilika."

Mzazi: "Naamini hivyo. Nitakagua daftari lake kila jioni."

Saikolojia inaeleza kuwa mtoto anayeona mzazi wake anathamini elimu na kuheshimu walimu hujifunza kuwa na nidhamu na kujituma. Hii ni kwa sababu watoto hufuata kile wanachokiona, si kile wanachoambiwa tu. Mfumo huu wa kushirikiana kati ya walimu na wazazi ni msingi wa mafanikio ya mwanafunzi, hasa katika mazingira ya vijijini ambako shule ni sehemu pekee ya elimu rasmi.

1.4: Matarajio ya Jamii kwa Mwanafunzi.

Katika jamii nyingi za Kiafrika, shule huchukuliwa kama njia ya kupambana na umasikini. Hivyo basi, mwanafunzi huonekana kama mwokozi wa familia yake. Matarajio haya yanamweka mwanafunzi katika hali ya shinikizo la kiakili, ambapo anahisi kwamba anapaswa kufaulu kwa gharama yoyote. Katika baadhi ya jamii kama Wasukuma, mtoto anayefanya vizuri shuleni hupewa heshima ya kipekee na jamii. Lakini hali hii pia huweza kumfanya mtoto wa familia masikini kuhisi aibu au kutengwa, hasa pale anaposhindwa kutimiza matarajio hayo.

“Mazungumzo kati ya mama na mwanae kuhusu umuhimu wa shule kwa maiha ya fanmilia yao”

Mwanafunzi: "Mama, mbona unanipigia kelele kila siku kuhusu kusoma?"

Mama: "Kwa sababu wewe ndiye tumaini letu. Ukianguka, familia nzima itaendelea kuteseka."

Mwanafunzi: "Lakini nahisi kama sitoshi. Shule ni ngumu sana."

Mama: "Tutasaidiana. Cha msingi ni kujitahidi na kuomba msaada kwa walimu."

Watoto wanaolelewa kwenye mazingira ya matarajio makubwa bila msaada wa kihisia hujikuta wakipatwa na msongo wa mawazo (stress). Tafiti zinaonyesha kuwa watoto wa umri wa miaka 10 hadi 14 wana uwezo mkubwa wa kujifunza, lakini pia ni rahisi kuvunjika moyo wanapokosea. Kwa hiyo, ni muhimu jamii iendelee kuwa na matarajio makubwa, lakini iyasawazishe na msaada wa kisaikolojia kwa watoto.


SURA YA 2: TABIA ZA WANAFUNZI WENYE NIDHAMU.

2.1: Maadili na Nidhamu Bora Darasani
Mwanafunzi mzuri hutambulika kwa tabia njema na nidhamu yake ya ndani inayodhihirika kwa nje. Hii ni pamoja na kuwasili shuleni mapema, kuheshimu walimu, kuepuka fujo, na kufuata sheria za shule. Tabia hii mara nyingi hujengwa tangu mtoto akiwa mdogo nyumbani. Kwa mfano, mtoto wa kabila la Wachaga ambaye huamshwa mapema kwenda shambani, ana tabia ya kuamka mapema hata shuleni, jambo linalomwezesha kufika mapema na kuwa tayari kwa masomo. Kisaikolojia, watoto wa umri wa kati ya miaka 7 hadi 12 hujifunza kwa kuiga zaidi (observational learning), hivyo wakiwa na wazazi au ndugu waliowajibika, wao pia hufuata mienendo hiyo.

“Mazungumzo  kati ya wanafunzi wawili na mwalimu”

Mwanafunzi A: "Mbona wewe huwa unakaa kimya darasani wakati wengine wanazungumza hovyo?"
Mwanafunzi B: "Bibi yangu alinifundisha kuwa ukimya ni hekima, na mwalimu anapaswa kusikilizwa."
Mwalimu: "Sawa kabisa. Hiyo ni tabia bora. Inaleta heshima na utulivu darasani."

Watoto wanaoishi kwenye familia zenye maadili thabiti hukua wakiwa na msimamo wa kimaadili. Hata hivyo, hata watoto waliotoka kwenye familia zisizo na misingi hiyo wanaweza kujifunza nidhamu kupitia walimu na marafiki wema. Mazingira ya shule yanapowekwa vizuri, yanaweza kumfanya mtoto kubadilika na kuwa na tabia njema.

2.2: Kushiriki katika Masomo na Shughuli za Shule.

Mwanafunzi mzuri hushiriki kikamilifu darasani – huuliza maswali, hutoa maoni, na hushiriki mijadala ya kielimu. Hali hii inaonyesha kwamba ana ari ya kujifunza na kuthamini elimu. Pia mwanafunzi huyu hushiriki michezo, klabu, na shughuli za kijamii kama usafi wa mazingira au uchoraji. Katika baadhi ya makabila kama Wamakonde, sanaa na uchoraji ni sehemu ya maisha ya kila siku, hivyo watoto wao huonyesha vipaji shuleni. Kisaikolojia, mtoto anaposhirikishwa katika shughuli mbalimbali hujenga hali ya kujiamini (self-efficacy) na uwezo wa kushirikiana na wenzake.

“Mazungumzo kati ya mwalimu na kija akiwa na rafiki yake”

Mwalimu: "Asanteni kwa kushiriki somo la leo. Lakini Kija alionesha bidii ya kipekee."
Kija: "Nilijiandaa tangu jana, Mwalimu. Nilivutiwa na mada ya historia ya Afrika."
Mwanafunzi mwingine: "Mimi natamani nifanane na Kija. Anaonesha kuwa elimu ni muhimu."

Hali ya mwanafunzi kushiriki huimarika zaidi anapopata usaidizi kutoka nyumbani. Wazazi wanaohakikisha watoto wao wanamaliza kazi za nyumbani, kuleta vifaa vya shule na kuwahimiza kushiriki, hujenga msingi wa maendeleo endelevu ya mtoto.

2.3: Heshima kwa Walimu na Wanafunzi Wengine.

Tabia nyingine muhimu ya mwanafunzi mzuri ni kutoa heshima kwa walimu na wanafunzi wenzake. Heshima ni msingi wa mahusiano bora shuleni. Mwanafunzi anapowasalimia walimu, kuepuka lugha chafu na kujua mipaka kati ya mchezaji na mfundishaji, hujenga mazingira salama na yanayohamasisha kujifunza. Kwa mtoto wa kabila la Waha, ambapo heshima kwa wakubwa ni jambo la msingi, mwanafunzi hujifunza mapema namna ya kuzungumza na watu kwa staha – tabia hii huambatana naye hata akiwa shuleni.

“Mazungumzo kati ya mwalimu na mwanafunzi kuhusu umuhimu wa kuomba ruhusa kabla  ya kuingia ndani”

Mwanafunzi: "Samahani Mwalimu, naweza kuingia?"
Mwalimu: "Karibu, na asante kwa heshima. Unajua si wote hukumbuka kuomba ruhusa."
Mwanafunzi mwingine: "Nitaanza kufanya hivyo pia. Najua itanisaidia hata nje ya shule."

Kitaalamu, watoto wanaopokea upendo lakini pia mipaka nyumbani hujifunza kuheshimu mamlaka. Hii inasaidia kujenga nidhamu ya ndani na tabia ya kujizuia kufanya mambo mabaya hata wakiwa peke yao. Heshima si tu kwa walimu bali pia kwa wanafunzi wenzake, haijalishi anatoka kabila gani au familia ipi.

2.4: Nidhamu ya Kujitambua na Kujiongozi.

Wanafunzi wema hujitambua – wanajua nguvu zao na udhaifu wao. Hawa ni wale wanaojua muda wa kusoma, muda wa kupumzika, na muda wa kucheza. Hawahitaji kusukumwa kila wakati kufanya kazi au kujifunza. Tabia hii ya kujiongoza hujengwa kutokana na malezi ya kimaadili, uzoefu wa maisha, au ushauri wa mara kwa mara kutoka kwa watu wazima. Kwa watoto wa kabila kama Wagogo, ambao hufundishwa kujitegemea mapema, tabia ya kujiongoza huonekana mapema shuleni.

"Mazungumzo kati ya mwalimu na muna"

Mwalimu: "Muna, ni nani aliyekukumbusha uje na ripoti ya utafiti mapema?"
Muna: "Hakuna mwalimu. Niliiandaa mwenyewe usiku. Najua kazi ni wajibu wangu."
Mwalimu: "Hongera. Hii ni tabia ya mwanafunzi bora kabisa."

Kulingana na saikolojia ya maendeleo, watoto wanaopata motisha ya ndani (intrinsic motivation) huonesha kiwango kikubwa cha kujitegemea na mafanikio darasani. Kujitambua ni msingi wa ubora katika taaluma na maisha kwa ujumla. Wanafunzi wanaopata nafasi ya kujipanga na kupanga ratiba zao hujifunza kutegemea juhudi zao wenyewe.

2.5: Faida za Kuwa Mwanafunzi Mzuri

Faida za kuwa mwanafunzi mzuri ni nyingi na hazipo tu ndani ya shule bali huendelea hadi utu uzima. Mwanafunzi mzuri huaminika, huteuliwa kuwa kiongozi wa darasa, anapewa nafasi ya kushiriki mashindano ya kitaaluma na hata hupata rufaa nzuri kutoka kwa walimu. Zaidi ya hayo, mwanafunzi huyu hupata marafiki wengi na kusaidiwa na jamii kwa haraka. Katika jamii kama ya Wanyakyusa, mtoto mwenye tabia njema hupewa fursa zaidi za msaada katika familia na hata jamii, kwa sababu huonekana kuwa na matumaini ya mafanikio.

“Mazungumzo kati ya mwalimu na Mwl mkuu wa shule kuhusu kumpata mwanafunzi mwenye nizamu kuiwakilisha shule”:

Mwalimu Mkuu: "Tunatafuta mwanafunzi wa kuwakilisha shule kwenye kongamano la kitaifa."
Mwalimu: "Tuweke jina la Deotila. Ameonesha nidhamu, bidii na busara katika kila jambo."
Mwalimu Mkuu: "Hapo sawa. Mwanafunzi mzuri daima hujifungulia milango yenyewe."

Pia, mwanafunzi mzuri anapomaliza shule, anabeba kumbukumbu chanya zinazomsaidia kupata fursa za ajira, uongozi au hata ufadhili wa masomo. Hii ni kwa sababu shule ni mahali ambapo tabia njema huonekana kwa vitendo – na dunia huthamini hilo. Kwa hiyo, kuanza kuwa mwanafunzi mzuri sasa ni uwekezaji kwa maisha ya baadaye.


SURA YA TATU

 TABIA ZA WANAFUNZI WASIO NA NIDHAMU

3.1: Dalili za Tabia Mbaya kwa Wanafunzi

Tabia za wanafunzi wasio na nidhamu hujitokeza kwa namna nyingi. Dalili za awali ni pamoja na kutofika shule kwa wakati, kuruka madarasa, kutofanya kazi za nyumbani, na kuongea ovyo darasani. Wanafunzi wengine hujionyesha kwa kuwatukana walimu au wenzake, kushirikiana na makundi mabaya, au kuvuruga

utulivu wa darasa. Tabia hizi huweza kuwa na chanzo kutoka nyumbani, hasa pale mzazi au mlezi hajali mwenendo wa mtoto. Kwa mfano, mtoto anayeishi na wazazi wenye ugomvi wa mara kwa mara nyumbani, huingia shuleni akiwa na hasira au kukosa utulivu wa kiakili. Katika baadhi ya jamii kama ya Wazaramo au Wangindo, watoto hulelewa na jamaa wa karibu, jambo linalofanya

usimamizi wa tabia uwe mdogo. 


“Mwalimu akimtia moyo petro kuhusu anayopitia nyumbani” 

Mwalimu: "Kila siku unatoka darasani bila ruhusa, Petro. Kitu gani kinakusumbua?" 

Petro: "Mwalimu, nyumbani hakuna amani. Baba huwa analeta wake wengine, mama hulia sana." 

Mwalimu: "Ninaelewa. Tutazungumza na mshauri wa shule. Usiogope, tuko pamoja." 

Kisaikolojia, watoto wanaokosa utulivu wa kisaikolojia nyumbani huwa katika hatari ya kutafuta njia mbadala za kutuliza huzuni au hasira zao, na mara nyingi  huonyesha hali hiyo kwa njia ya vurugu au ukaidi. Tabia hizi huchangiwa pia na marafiki wabaya, ambao huwashawishi wenzao kufanya makosa ili kujionesha “wanaume” au “wajanja”.


3.2: Chanzo cha Tabia Mbaya Shuleni

Chanzo kikuu cha tabia mbaya shuleni ni mazingira yasiyomuandaa

mwanafunzi kimaadili na kihisia. Watoto wanaokua bila uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi, walimu au jamii, hujikuta wakijenga tabia za kupinga mamlaka, kudharau wengine na hata kuiba. Kwa watoto wa jamii za wafugaji kama Wamaasai, ambapo uhuru wa mtoto hupewa kipaumbele zaidi ya nidhamu ya kikanuni, mtoto anaweza kushindwa kuelewa umuhimu wa kufuata ratiba na

sheria za shule. Hii haimaanishi kabila hilo ni lenye tabia mbaya, bali mazingira ya kijamii na mila vinaweza kuchangia kutokuwepo kwa utaratibu wa kuelewa sheria za shule. 


"Mazungumzo kati ya mwalimu na mwanafunzi:"

Mwanafunzi: "Mwalimu, kwetu sisi mtoto huamua mwenyewe

kama anasoma au hapana." 

Mwalimu: "Ndiyo, lakini hapa shule tunajifunza kuwajibika na kuheshimu ratiba." 

Mwanafunzi: "Sawa mwalimu nimekuelewa. Nitajitahidi nizoe." 

Kulingana na nadharia ya Maslow ya mahitaji ya binadamu, mtoto anahitaji kutoshelezwa kimwili na kihisia kwanza ili aweze kujifunza vizuri. Pale ambapo mtoto hana chakula, nguo, au upendo, akili yake hushindwa kutulia kwenye masomo au sheria za shule. Badala yake, huelekeza nguvu kwenye kutafuta hisia za kukubalika hata kwa njia mbaya. 


3.3: Athari za Tabia Mbaya kwa Elimu na Maisha.

Tabia mbaya huathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma na  kijamii. Mwanafunzi wa aina hii hushindwa kumaliza kazi za shule, hupata alama za chini, na hatimaye kupoteza motisha ya kuendelea na elimu. Zaidi ya hapo, tabia mbaya huathiri mahusiano yake na walimu na wanafunzi wengine. Hali hii husababisha kujitenga au kutengwa, na kupelekea hali ya msongo wa mawazo (stress) au hata kupoteza mwelekeo wa maisha. Kwa mfano, mtoto wa jamii ya Wanyamwezi, anayekuzwa kwa misingi ya kujichanganya kijamii, anaweza kupatwa na huzuni kubwa anapojikuta akitengwa kutokana na tabia mbaya. 

“Mazungumzo kati ya mwalimu na mwanafuzi kuhusu makele ya mwanafunzi akiwa mazingira shule” 

Mwanafunzi: "Mwalimu, kwa nini hamnipendi kama wengine?"

Mwalimu: "Si kwamba hatukupendi. Ila unahitaji kubadilika. wengine wanashindwa hata kujifunza kwa sababu ya kelele zako."

Mwanafunzi: "Sawa mwalimu. Nataka kubadilika lakini siwezi peke

yangu.” 

Mwalimu: "kuanzia leo utakuwa unashirikiana na Eliza ili ujifunze kutoka kwake tabia njema” 

Mwanafunzi: :Sawa mwalimu na ahsante pia nitafanya hivyo , sitakuangusha kwenye hili” 

Kulingana na tafiti za kisaikolojia, wanafunzi wasio na nidhamu mara nyingi hupitia changamoto za kutokueleweka, ukosefu wa msaada wa kiakili au ugumu wa kueleza hisia zao. Hii huwafanya kuonekana wabaya, lakini ndani yao kuna kilio cha kuhitaji msaada. Tabia mbaya ni matokeo ya kutokupewa nafasi ya kujieleza au kutokuwa na msaada sahihi. 


3.4: Ushawishi wa makundi rika 

Makundi rika yana athari kubwa kwa tabia ya mwanafunzi. Wanafunzi wengi hujiingiza kwenye tabia mbaya si kwa sababu walitaka, bali walishinikizwa na marafiki ili waonekane “wanafit” kwenye kundi fulani. Ushawishi huu unaweza kuwa wa kutumia lugha chafu, kuiba, kutoroka shule, au hata kutumia dawa za

kulevya. Katika makabila ya kijijini kama Wakwere, mtoto anapohamia shule za mjini  hukutana na changamoto mpya zisizofanana na zile za nyumbani. Kukosa msaada wa ufuatiliaji kutoka kwa wazazi au ndugu, mtoto huyu hukubali mashinikizo ya marafiki haraka ili kujihisi salama. 


“Mazungumzo kati ya wanafunzi wawili wakiume wakipanga kutoroka“ 

Mwanafunzi A: "Si unajua tukitoroka kesho tutakutana uwanjani? Wanaume wa kweli hawabaki shuleni!"

Mwanafunzi B: "Lakini tutaadhibiwa. Naogopa kusema kweli."

Mwanafunzi A: "Usiwe mwoga. Ukikataa, hutakuwa rafiki yetu

tena." 

Mwanafunzi B:“Kama urafiki wenyewe ndio huu, kuanzia leo

kilamtu afanye mambo yake” 

Saikolojia inaeleza kuwa wakati wa ujana, hamu ya kukubalika na kundi ni kubwa sana kuliko hata kupendwa na mzazi au mwalimu. Hali hii huweka watoto kwenye hatari ya kukubali kufanya mambo mabaya ili kuendana na wenzake. Watoto wasio na uwezo wa kusema “hapana” huwa katika hatari zaidi ya kuwa na tabia mbaya. 


3.5: Ushahidi wa matukio halisi Mashuleni 

Katika shule nyingi, walimu wamekuwa wakishuhudia mabadiliko hasi kwa baadhi ya wanafunzi kutokana na tabia mbaya. Mfano halisi ni mtoto mmoja aliyehamia kutoka kijiji cha mbali hadi mjini kwa masomo ya sekondari. Akiwa  darasa la kwanza alikuwa mpole na mwenye bidii, lakini baada ya mwaka mmoja alianza kuonyesha ukaidi, kutukana walimu na kuiba vifaa vya wanafunzi. Baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa mtoto huyu alikuwa akiishi

kwa ndugu ambao walimpuuza na kumwachia ajitunze mwenyewe. Mabadiliko haya yalichangiwa na ukosefu wa upendo, usimamizi na mazingira mapya ya mji.

“Mazungumzo kati ya mwalimu mkuu na mwalimu wa darasa

mabadiliko ya tabia ya mtoto” 

Mwalimu Mkuu: "Mtoto huyu alikuwa na nidhamu nzuri mwaka jana. Nini kimetokea?"

Mwalimu wa darasa: "Anakaa kwa mjomba wake lakini anaonekana

kuwa hana uangalizi wowote. Marafiki zake wengi ni wavulana

wasumbufu wa mtaani." 

Mwalimu Mkuu: "Tutamwita na tumshirikishe mshauri wa shule na walezi wake.

" Matukio kama haya huonyesha kuwa hakuna mwanafunzi mbaya kwa asili. Tabia zote hufundishwa na kuathiriwa na mazingira. Kwa hiyo, badala ya kuhukumu mwanafunzi mara moja, jamii nzima ya shule walimu, wazazi, viongozi wa dini na wanafunzi wenzake – inapaswa kushirikiana kumsaidia kurejea katika njia sahihi.


SURA YA 5.

JINSI WALIMU WANAVYOISHI NA WANAFUNZI  WASUMBUFU

5.1: Walimu hupoteza subira kwa haraka
Wanafunzi wasumbufu mara nyingi hukumbana na hasira ya walimu. Walimu wengi hupoteza subira pindi mwanafunzi anapokataa kufuata maelekezo, kuchelewa darasani, au kutohudhuria masomo. Tabia hizi huwachosha walimu na kuwafanya kutoa adhabu bila kuchunguza chanzo. Kisaikolojia, mwalimu aliyekabiliwa na msongo wa kazi na idadi kubwa ya wanafunzi huathiriwa kiakili, hivyo kushindwa kuvumilia mienendo ya hovyo darasani. Kwa mfano, mtoto wa jamii ya Wamakonde anayekuzwa kwa uhuru mwingi nyumbani huleta tabia hizo shuleni, ambazo kwa mwalimu zinaonekana kama ukaidi.
Published from Blogger Prime Android App

“Mazungumzo kati ya mwalimu na mwanne kuhusu tabia yake ya kuja na simu shuleni”

Mwalimu: "Mwanne, mara ngapi nimesema usilete simu darasani?"
Mwanne: "Samahani Mwalimu, nilisahau kuiacha  nyumbani."
Mwalimu (kwa hasira): "Kama huna adabu nyumbani, usinilite hapa. Toka nje sasa hivi!"

Hasira za walimu zinapotolewa mara kwa mara, hujenga uadui kati ya mwanafunzi na mwalimu. Badala ya kusaidia kurekebisha tabia, mwanafunzi anajiona hana nafasi ya kueleweka. Hii huongeza utovu wa nidhamu. Walimu wanashauriwa kutumia njia za kuelewa sababu za tabia mbaya kabla ya kuchukua hatua.

5.2: Walimu Hutoa adhabu kali kwa haraka
Adhabu zinazotolewa kwa wanafunzi wasumbufu mara nyingi huwa kali na za ghafla—kupigwa viboko, kufukuzwa darasani au hata kufungiwa masomo. Walimu wengi huamini kuwa adhabu ndicho kifaa bora cha kurekebisha tabia. Hata hivyo, tafiti za kisaikolojia zinaonesha kuwa adhabu ya mwili husababisha hofu badala ya mabadiliko ya tabia. Watoto walio na matatizo ya kiakili au wanaotoka familia zenye migogoro hushindwa kuelewa kosa lao, bali hujenga uasi wa ndani.

“Mazungumzo kati ya mwanafunzi na mwalimu”,

Mwanafunzi: "Mwalimu, mbona umenipiga mimi peke yangu ilhali wote tulikuwa tunazungumza?"
Mwalimu: "Wewe ndiyo unasumbua zaidi. Na utaendelea kupigwa mpaka uache."
Mwanafunzi (kwa huzuni): "Sioni haja ya kuja shule tena kama ni mateso tu."
Katika jamii kama ya Wairaq, watoto hufundwa kwa njia ya maelezo na kushirikishwa, si kwa adhabu kali. Shule zinapofuata mfumo wa adhabu badala ya mazungumzo, hushindwa kusaidia mwanafunzi kuelewa makosa yake. Walimu wanapaswa kupewa mafunzo ya elimu ya saikolojia ya mtoto ili kutumia mbinu mbadala kama ushauri au mashauriano.

5.3: Walimu hupunguza matumaini kwa mwanafunzi mzuri kutoka kwa wasumbufu.

Wanafunzi wasumbufu mara nyingi huonekana kama watu wasio na matumaini. Walimu huweza hata kusema mbele ya darasa, "Wewe huwezi kufaulu!" au "Wewe ni mzigo tu." Matamshi haya huumiza sana na kushusha ari ya kujifunza. Kulingana na saikolojia ya ukuaji, watoto wa umri wa miaka 10 hadi 15 wako katika hatua ya kutafuta utambulisho. Matamshi ya kukatisha tamaa kutoka kwa watu wazima hujenga picha hasi ya nafsi (negative self-image). Katika baadhi ya jamii kama ya Wakurya, mtoto anapokataliwa au kubezwa, hujenga chuki ya ndani ambayo hupelekea uhalifu au utoro.

“Mazungumzo ya mwalimu akimkatisha tamaa mwanafunzi”
Mwanafunzi: "Mwalimu, nilijitahidi kwenye mtihani huu, nimepata 45%."
Mwalimu: "Wewe hata ukipewa mitihani mitupu hutafaulu. Bora uache shule."
Mwanafunzi (kimya, akitoka kwa huzuni): "Labda kweli sifai."
Maneno ya kukatisha tamaa huumiza zaidi kuliko adhabu ya mwili. Walimu wanapaswa kujifunza kutumia lugha ya kutia moyo hata kwa mwanafunzi mwenye tabia mbaya. Kwa kufanya hivyo, huchochea mabadiliko chanya.

5.4: Walimu Huwatenga Wanafunzi Wasumbufu.
Mara nyingi wanafunzi wasumbufu huwekwa pembeni, hawapewi nafasi ya kushiriki darasani, hawateuliwi kwenye kazi za kikundi, na hata hutengwa kwenye shughuli za kijamii. Kutengwa huku hupelekea mwanafunzi kuwa mpweke, na mpweke hujenga hasira au uasi wa ndani. Kisaikolojia, watoto walio na tabia mbaya mara nyingi wanatafuta uangalizi (attention-seeking behavior). Kutengwa huongeza hitaji hilo na kwa kawaida hujitokeza kwa tabia mbaya zaidi. Katika jamii kama ya Wamasai, mtoto asiyepewa nafasi ya kuonyesha uwezo wake hujihisi asiye na thamani.

“Mazungumzo kati ya mwalimu na mwanafunzi, mwalimu akimkatisha tamaa mtoto”

Mwanafunzi: "Mwalimu, naweza kushiriki kwenye kikundi cha uchoraji?"
Mwalimu: "Wewe? Huko si kwa wavivu kama wewe. Kaa mbali!"
Mwanafunzi kwa hasira: "Basi sitafanya kitu chochote!"
Badala ya kuwatenga, walimu wanashauriwa kuwapa wanafunzi hao nafasi maalum ya kuonyesha vipaji vyao iwe ni michezo, sanaa, au kazi za mikono. Hii huwasaidia kujiona kuwa na thamani, hivyo kubadili mwenendo.

5.5: Walimu wachache hujaribu kuelewa sababu za tabia mbaya.

Ingawa walimu wengi huadhibu au kutenga wanafunzi wasumbufu, wachache hujaribu kufahamu kwa undani sababu za tabia hizo. Wengine huwaita wazazi, kuzungumza nao au kuwapa ushauri binafsi. Njia hii mara nyingi huzaa matunda. Kwa mfano, mwanafunzi wa jamii ya Wazaramo aliyekosa chakula nyumbani anaweza kuonekana mvivu shuleni, kumbe ana njaa au huzuni. Mwalimu anayejua hili anaweza kubadili maisha ya mwanafunzi huyo. Kisaikolojia, mtoto anayejaliwa na kueleweka huanza kubadilika na kuwa mtulivu zaidi.

“Mazungumzo kati ya mwalimu na kassimu kushusu u”

Mwalimu: "Kassim, mbona siku hizi unaonekana huna furaha na unazubaa darasani?"
Kassim: "Mwalimu, baba alifariki mwezi uliopita. Hali nyumbani ni ngumu sana."
Mwalimu (kwa huruma): "Pole sana Kassim. Njoo tuongee baada ya darasa. Tupo pamoja."

Uelewa wa walimu unahitajika zaidi katika kusaidia wanafunzi wasumbufu. Shule bora ni ile inayochunguza mzizi wa tatizo badala ya kulitibu juu juu kwa hasira au adhabu. Hii ndiyo njia ya kuwatengeneza wanafunzi wa kesho.


SURA YA 6: ATHARI ZA MATENDO YA WALIMU KWA WANAFUNZI

6.1: Kuongezeka kwa hofu na msongo wa mawazo.

Matendo ya walimu, hasa pale wanapotoa adhabu zisizo na maelezo, matamshi ya kuudhi, au unyanyapaa, hujenga hofu ya ndani kwa wanafunzi. Hofu hii husababisha msongo wa mawazo, kushuka kwa uwezo wa kujifunza, na hatimaye kupoteza mwelekeo wa kitaaluma. Kulingana na saikolojia ya ukuaji, watoto wa miaka 11–16 wako katika kipindi cha kujitambua; hivyo, matamshi hasi kutoka kwa walimu huwa na athari kubwa kwa nafsi zao. Wanafunzi kutoka jamii zinazozingatia heshima na utulivu kama ya Wasambaa, wanapoonyeshwa ukali kupita kiasi, hukosa ujasiri wa kuuliza maswali au kushiriki darasani.

"Mazungumzo kati  ya mwanafunzi mwalimu"

Mwanafunzi: “Mwalimu, ningependa kuuliza swali, lakini niliwahi kuambiwa na mwalimu mmoja kwamba mimi ni mjinga.”
Mwalimu Mwingine: “Samahani kwa aliyesema hivyo. Hapa darasani, hakuna swali la kijinga. Uliza kwa uhuru.”
Mwanafunzi (akiwa na woga bado): “Ni vizuri kusikia hivyo, ila bado naogopa kukosea.”

Hofu kama hii husababisha mwanafunzi kushindwa kuonyesha uwezo wake halisi. Walimu wanapaswa kujua kuwa maneno yao ni kama mbegu yanaweza kukuza au kuharibu kabisa maisha ya mtoto.

6.2: Kujenga chuki na uasi.

Pale walimu wanapowatendea wanafunzi kwa dharau, ukatili au upendeleo, wanafunzi hujenga chuki ya ndani, ambayo hubadilika kuwa uasi wa wazi au wa kimya kimya. Uasi huu huweza kuonekana kwa vitendo kama kutotii sheria za shule, utoro, au hata uharibifu wa mali za shule. Kisaikolojia, mtoto aliyejeruhiwa kihisia mara nyingi hulipiza kisasi kwa njia ya tabia isiyofaa. Kwa jamii kama ya Wakwere, ambapo watoto hufundwa kwa mazungumzo na maonyo ya heshima, wanapokutana na ukatili mashuleni, huona shule kama adui.

"Mazungumzo kati ya mwalimu mkuu na mlinzi wa shule"

Mwalimu Mkuu: “Mbona kijana huyu anaharibu vioo vya madarasa kila wiki?”
Mlinzi wa shule: “Asema mwalimu wake humtukana mbele ya wenzake. Anaona kama hii shule ni adhabu kwake.”
Mwalimu Mkuu: “Lazima tumshirikishe mshauri wa wanafunzi na mzazi wake kabla mambo hayajazidi.”

Uasi unaoanzia shuleni huendelea hadi utu uzima. Ni wajibu wa walimu kutengeneza mazingira ya heshima ili kuzuia mabadiliko hasi ya tabia.

6.3: Kujenga au kuua ndoto za wanafunzi.

Mwalimu ana uwezo wa kujenga ndoto za mwanafunzi, au kuzivunja kabisa. Kauli ndogo kama “Unaweza kuwa daktari” au “Wewe huwezi hata kuwa makarani” huweza kubadilisha maisha ya mwanafunzi. Katika makabila kama ya Wachaga, ambapo watoto hupewa shinikizo kubwa la mafanikio, walimu wanapowakatisha tamaa, huongeza mzigo wa kihisia. Kisaikolojia, mtoto anayetiwa moyo hujenga picha chanya ya maisha na kupambana kufikia ndoto zake.

"Mazungumzo kati ya mwalimu na mwanafunzi"

Mwanafunzi: “Mwalimu, nilipata 30% kwenye Hisabati, lakini nataka kuwa mhandisi.”
Mwalimu: “Hilo ni lengo zuri. Tutatengeneza ratiba ya masomo ya ziada na kukusaidia.”
Mwanafunzi: “Asante sana. Nilitaka kuacha ndoto hiyo, lakini sasa najisikia naweza.”
Mazingira ya shule yenye walimu wanaotia moyo hujenga kizazi cha watu jasiri na wanaojiamini. Ndoto ni rahisi kuua, lakini kugumu kuzitengeneza tena. Hili linapaswa kuzingatiwa sana.

6.4: Kuathiri Uhusiano wa Kijamii wa Mwanafunzi.

Tabia ya mwalimu kwa mwanafunzi huweza kuathiri hata uhusiano wake na wanafunzi wenzake. Wanafunzi wanaopendelewa au kubezwa hujenga uhusiano wa chuki, wivu, au dharau kati yao. Kwa mfano, mwanafunzi anapoitwa “mpumbavu” mbele ya wengine, anakuwa kituko cha darasa. Kisaikolojia, hii hujenga hali ya kujitenga (social withdrawal), ambapo mtoto hukataa kushirikiana, kuzungumza, au kushiriki michezo ya pamoja. Hili ni hatari zaidi kwa jamii zinazokuza mshikamano kama ya Wanyakyusa.

"Mazungumzo kati ya wanafunzi wawili" 

Mwanafunzi 1: “Mwalimu anasema wewe huwezi hata kuandika vizuri. Unachekesha.”
Mwanafunzi 2 (kwa huzuni): “Naona bora nisihudhurie darasa lake kabisa. Sijisikii salama.”
Mwanafunzi 1: “Tusiwe hivyo. Acha nikusaidie tujikumbushe tulichojifunza jana.”

Uhusiano mzuri wa kijamii hujengwa kwa mazingira ya heshima na uelewano. Mwalimu ndiye kiongozi wa jamii ya darasani, hivyo anatakiwa kuonesha mfano mzuri.

6.5: Kuathiri Maamuzi ya Baadaye ya Mwanafunzi.

Tabia ya walimu kwa wanafunzi huathiri hata maamuzi yao ya baadaye. Mwanafunzi aliyeshushwa hadhi au kunyanyaswa huweza kuamua kuacha shule, kutojiunga na taasisi yoyote ya elimu, au hata kuwa na mtazamo mbaya juu ya walimu milele. Kwa upande mwingine, mwanafunzi aliyelelewa kwa busara huendelea kuwa na heshima kwa elimu, hata kama alikutana na changamoto. Katika familia nyingi za Kiafrika, mtoto huchukulia mwalimu kama mzazi wa pili. Pale ambapo “mzazi” huyu humtendea vibaya, mwanafunzi hupoteza dira.

"Mazungumzo kati ya mwalimu wa zamani na mwalimu wa mpya"

Mwanafunzi wa zamani: “Nilikatisha masomo kwa sababu mwalimu aliniambia sina akili kabisa.”
Mwalimu mpya: “Pole sana. Lakini bado una nafasi. Kuna kozi za jioni unaweza anzia tena.”
Mwanafunzi: “Kwa kweli ningeambiwa haya mapema, nisingepoteza muda wangu wote mitaani.”

Hii inaonesha kuwa matendo ya walimu yanavuka mipaka ya darasa na kugusa maisha ya baadaye ya wanafunzi. Walimu wanatakiwa kuacha kumbukumbu chanya kwenye maisha ya kila mwanafunzi anayewapitia.

Jipatie kitabu hiki kupitia

Download full hapa 👇


https://selar.com/m/daniel-ndisa1


0 Comments:

Advertisement