Saturday, February 1, 2025

MJENGO WA TUNGO KATIKA KISWAHILI

MJENGO WA TUNGO KATIKA KISWAHILI
Tungo ni kipashio cha kisarufi kilichoundwa kwa kuunganisha pamoja vipashio vidogovidogo vilivyo chini yake. Au Tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili. 
>Tungo hujengwa na vipashio vidogovidogo kama vile mofimu kuunda neno, neno kuunda kirai, kirai kuunda kishazi na kishazi kuunda sentensi.Kwa kawaida tungo huanzia neno.

AINA ZA TUNGO
Tungo neno: Tungo neno ni tungo ambayo huundwa na vipashio vidogo zaidi ya neno ambayo ni mofimu au fonimu.
Mfano;anacheza, kakimbia

Tungo kirai:Ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi lakini ambacho hakina Muundo wa kiima na kiarifu.
Mfano; mtoto mweusi, kiyama chale, bondeni

Tungo kishazi:Ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe. 

KIRAI NA UAINISHAJI WAKE
Dhana ya kirai itaeleweka kwa kuzingatia sifa zake zifuatazo

  1. Kirai huwa ni kipashio cha kimuundo kisichokamilika yaani hakina Muundo wa kiima na kiarifu
  2. Kirai huainishwa kimuundo kulingana na neno kuu la kirai husika
  3. Kirai ni tungo,yaani ni aina moja wapo ya tungo, aina nyingine za tungo ni neno, kishazi na sentensi.
  4. Kirai hudokeza maana, lakini maana hiyo si kamili
  5. Maneno katika kirai lazima yapangwe kimantiki kwa mpangilio unaokubalika katika sarufi ya lugha husika
MAKUNDI YA KIRAI 
  1. Kirai Nomino(KN);Ni kirai ambapo neno lake kuu ni nomino. Ni kirai ambacho Muundo wake umekitwa kwenye nomino na neno au mafungu ya maneno.
  2. Kirai kitenzi (KT);Ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi na neno au mafungu ya maneno. Hii inamaana neno lake kuu ni kitenzi.
  3. Kirai kivumishi(KV);Ni kirai ambacho Muundo wake umekitwa katika kivumishi. Muundo huu huwa ni wa kivumishi na neno au mafungu ya maneno linaloandamanacho.
  4. Kirai kielezi(KE); Tofauti na aina nyingine ya virai miundo ya virai vielezi haielekei kukitwa kwenye mahusiano ya lazima baina ya neno kuu (kielezi) na fungu la maneno linaloandamana nalo.
  5. Virai viunganishi (KU);Ni kirai ambacho Muundo wake umekitwa katika mahusiano baina ya kwa na katika, au kwenye na fungu la maneno.
TUNGO KISHAZI 
Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.

Sifa za kishazi
  1. Kishazi hupatikana katikati/ndani ya sentensi
  2. Kishazi lazima kiwe na kitenzi, sehemu yoyote ya sentensi isiyo na kitenzi haiwezi kuwa kishazi.Kishazi huru hutawaliwa na kishazi kikuu na kishazi kitegemezi hutawaliwa na kishazi kitegemezi.
  3. Baadhi ya vishazi huweza kujitegemea kama sentensi hata vikiondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu. Kinachoweza kijisimamia kama sentensi huitwa kishazi huru kikiwa ndani ya sentensi kuu na huitwa "Sentensi sahili" kikiwa sentensi inayojitegemea.
  4. Baadhi ya vishazi haviwezi kujitegemea kama sentensi ikiwa vitaondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu
  5. Vishazi vingi hata vishazi huru huwa na kiima dhahiri
  6. Kishazi kwa kawaida hasa kishazi huru huwa na kitenzi kimoja huru.
  7. Kitenzi hicho huweza kuandamana na kitenzi kisaidizi, pia kitenzi katika kishazi huweza kuwa kitenzi kishirikishi.
  8. Kishazi hutekeleza majukumu mbalimbali ya kisarufi
  9. Tofauti ya kishazi na sentensi ni kwamba kishazi hupatikana ndani ya sentensi lakini sentensi hujisimamia kimuundo na kimaana. Kishazi huwa na kiarifu kimoja na kiima kimoja, lakini sentensi huweza kuwa na kiima kimoja
AINA ZA VISHAZI 
  1. Vishazi huru: Kishazi huru ni kishazi kinachotawaliwa na kitenzi kikuu ambacho kwa kawaida hutoa ujumbe kamili usio hitaji maelezo zaidi ya kukamilisha maana. Hivyo hata vikiondoshwa katika muktadha wa sentensi huweza kujitegemea kama sentensi.
  2. Vishazi vitegemezi: Kishazi kitegemezi ni kinachotawaliwa na kitenzi kisaidizi ambacho Muundo wake hukifanya kutegemea kitenzi cha kishazi huru ili kuweza kutoa ujumbe uliokusudiwa. Kishazi kitegemezi peke yake hakitoi ujumbe unaojitosheleza.
Sifa za kishazi kitegemezi
  1. Kishazi kitegemezi hutoa maana kamili kinapoandamana na kishazi huru
  2. Kishazi kitegemezi kinaweza kufutwa katika sentensi bila kuaribu maana ya sentensi nzima.
  3. Kishazi kitegemezi hutambulishwa na viambishi vya utegemezi vinavyoambatanishwa kwenye kitenzi
  4. Kishazi kitegemezi vile vile kinaweza kutambuliwa kwa kuwepo vishazi kama vile ingawa, kwamba,ili, kwa sababu,mzizi wa amba,mofu ya masharti nk.
Aina ya vishazi vitegemezi
a)vishazi tegemezi vivumishi
1.vishazi vitegemezi vinavyotokea pamoja na nomino inayovumishwa
2.Vishazi vitegemezi visivyoambatana na nomino inayovumishwa

b) Vishazi vitegemezi vielezi
1.vishazi tegemezi vya mahali
2.vishazi tegemezi vya wakati
3.vishazi tegemezi vya namna au jinsi
4.vishazi tegemezi vya masharti
5.vishazi tegemezi vya hali,hitilafu,

UFAFANUZI WA AINA ZA TUNGO
1.SENTENSI
Sentensi ni kifungu cha maneno kuanzia neno moja na kuendelea chenye Muundo wa kiima na kiarifu na kinacholeta maana kamili

Sifa za sentensi 
>Sentensi lazima iwe na mpangilio wa maneno ambao unakubalika na wazungumzaji wa lugha husika.

  1. sentensi lazima ikamilike kimaana, kimuundo, na kisarufi 
  2. Sentensi huwa na Muundo wa kiima na kiarifu/huwa na kirai Nomino na kirai kitenzi
  3. Sentensi huweza kuwa na zaidi ya kiima kimoja na kiarifu kimoja au zaidi
  4. Sentensi inaweza kuundwa na kitenzi kikuu kimoja au zaidi
  5. Sentensi inaweza kuundwa na kishazi huru kimoja au zaidi kishazi kitegemezi kimoja au zaidi
  6. Sentensi huonyesha hali mbalimbali kama vile amri, ombi, mshangao, swali n.k
Sentensi inakuwa na vipengele vifuatavyo. 
a)Kiima:Ni sehemu katika sentensi ambayo hujaza sehemu ya mtenda au mtendwa wa jambo linaloelezwa. Katika tungo kiima hutokea kushoto mwa kitenzi.

b) Kiarifu:Ni sehemu katika sentensi inayojazwa na maneno yanayo arifu tendo lililofanywa, linapofanywa, au litakapofanywa. Kiarifu ndiyo sehemu muhimu zaidi katika sentensi ambayo wakati mwingine huweza kusimama pekee, na wakati mwingine huchukua viwakilishi vya kiima.

AINA ZA SENTENSI

1.SENTENSI SAHILI
Ni sentensi ambayo huundwa na kishazi huru kimoja.sentensi ya aina hii huwa inaelezea taarifa moja tu.
Mfano
-wanafunzi wanafanya mtihani
-Walinzi walitaka kunizuia nisiingie ndani

Muundo wa sentensi sahili
1.muundo wa kitenzi kikuu(T) pekee.
mfano:Gari limeanguka
2.Muundo wa kitenzi kikuu (T) na kitenzi kisaidizi(Ts)
Mfano:Juma alitaka(Ts) nisipate (T) utajiri
3.Muundo wa vira-tenzi vilivyokitwa katika kitenzi "kuwa": mfano John amekuwa akiangalia Tv kwa muda mrefu sana
Muundo wa kitenzi kishirikishi
Mfano: Kiswahili ni tunu ya Taifa

Sifa za sentensi sahili 
  • .Ina kiima ambacho kimetajwa wazi au kimeachwa kutajwa kwa kuwa kinaeleweka
  • Ina kiarifu ambacho kimeundwa na kitenzi kikuu kimoja au kitenzi kikuu kisaidizi au kitenzi kishirikishi na kijalizo na chagizo.
  • Haifungamani na sentensi nyingine na hivi inajitosheleza kimuundo na kimaana

2.SENTENSI CHANGAMANO
Hii ni sentensi ambayo huundwa na kishazi huru kimoja au zaidi na kishazi kitegemezi kimoja au zaidi.
sifa kubwa ya sentensi changamano ni kuwa na kishazi kitegemezi ambacho hutegemea kishazi kingine huru ndani ya sentensi hiyo.Msingi muhimu wa uhusiano ndani ya sentensi hizo ni ule wa kishazi kimoja kutegemea kingine.
NB: Sentensi changamano ina Muundo wenye vishazi virejeshi.
Mfano:Gari lililopinduka jana jioni halikuharibika hata kidogo

3.SENTENSI AMBATANO

Ni aina ya sentensi ambayo huundwa kwa vishazi viwili au zaidi pamoja na kiunganishi hicho ndipo hufanya kazi ya kuunganisha vishazi Hivyo viunganishi ni kama vile lakini,wala,au,na,nk

MUUNDO WA SENTENSI AMBATANO( AMBATANI)
(i) sentensi sahili na sentensi sahili
Mfano: Baba analima na Mama anapanda
(ii) sentensi sahili na sentensi changamano
Mfano: mwalimu anafundisha lakini wanafunzi anaowafundisha wanacheza.
(iii) Miundo yenye sentensi changamano tu
Mfano:Barabara zilizojengwa na wakoloni zimedumu hadi leo wakati zile zilizojengwa na wachina hata mwezi hazifikishi.

4.SENTENSI SHURUTIA
Ni sentensi ambayo huundwa kwa mofimu za masharti kama vile kinge,ngali,pamoja na ngeli,asingali
Mfano:
-Juma angelisoma kwa bidii angelifahulu mitihani
 -Mwalimu angechelewa kidogo wanafunzi wangeumizana

Kwa mawasiliano juu ya matini ya kufundishia
             Whatsapp no 0768569349 tuma SMS usipige

0 Comments:

Advertisement