Saturday, February 15, 2025

UPIMAJI WA KIELIMU NA AINA ZAKE

UPIMAJI WA KIELIMU
Dhana ya Upimaji wa kielimu
Ni mchakato unaotumika katika kupata data na mabadiliko ambayo mwezeshaji huweza kujua uwezo na ujuzi wa mwanafunzi na mabadiliko ya kitabia.

Malengo ya Upimaji wa kielimu
(a) kuangalia kiwango ambacho malengo ya mada yamefikiwa na mwanafunzi
(b)kuamsha ari ya mwanafunzi kujifunza zaidi
(c)kumpa mwezeshaji dira ya kumwongoza katika kuboresha ufundishaji
(d)kusaidia katika uwekaji wa kumbukumbu za kila mwanafunzi
(e) kupata taarifa za mabadiliko katika stadi, ujuzi na mwenendo wa mwanafunzi

Umuhimu wa Upimaji
Katika elimu Upimaji wa maendeleo ya mwanafunzi hufanywa ili kujua maendeleo ya mwanafunzi na hasa kujua ni kiasi gani mwanafunzi amepata stadi na maarifa yatakayomwezesha kuishi maisha bora na kuwa na manufaa katika jamii anamoishi.

Umuhimu wa Upimaji wa maendeleo ya mwanafunzi
1.kumwezesha mwezeshaji kutoa uamuzi wa mafundisho ya kila siku.
2.kujua iwapo mitaala na ufundishaji unastahiri unakidhi mahitaji ya mwanafunzi ili kusaidia katika
Kuwapanga wanafunzi ili waweze kufundishwa kulingana na uwezo wao
Kujua kama wanafunzi wako tayari kwa mafunzo mapya
  • Kuonyesha maendeleo ya mwanafunzi kwa ujumla
  • Kuamsha ari ya wanafunzi katika kujifunza
  • Kutambua sehemu maalumu zinazohitaji kurudiwa
  • Kugundua matatizo au ugumu wanaoupata wanafunzi katika kujifunza
  • Kugundua wanafunzi ambao wako nyuma
  • Kuonyesha ubora au ubovu wa ufundishaji
  • Kujua kiasi ambacho mwanafunzi amemudu katika kupata stadi za lazima
3.Kumsaidia kuboresha ufundishaji
4.Kuonyesha uwajibikaji wa mwalimu na mwanafunzi
5.Kusaidia uchaguzi wa mwanafunzi na utoaji wa vyeti.

AINA ZA UPIMAJI WA MAENDELEO YA MWANAFUNZI
Zipo aina nne za Upimaji wa maendeleo ya mwanafunzi.Aina hizo ni:
  • Upimaji awali
  • Upimaji endelevu
  • Upimaji wa mwisho au tamati
  • Upimaji tatuzi
UPIMAJI AWALI
Upimaji wa aina hii humsaidia mwalimu kuelewa mahali ambapo mwanafunzi anapaswa kuanzia katika kujifunza.hivyo unapaswa kuzingatia nyanja zote za kielimu kama utambuzi, mwenendo na vitendo anavyomudu mwanafunzi anapoandikishwa shule.hapa unaweza andaa maswali ya kuwauliza mfano utaweka picha na kuwatawala waeleze wanachokiona katika picha na kumtaka mmoja mmoja ajibu.
Fomu ya Upimaji awali

UPIMAJI ENDELEVU
Upimaji wa aina hii hutolewa wakati mwalimu anaendelea kufundisha.mfano mwalimu anapofundisha mada fulani basi anaweza kutoa zoezi au jaribio kila baada ya kufundisha kipengele kimoja.upimaji huu unalenga kuona kama mwanafunzi amemudu kipengele hicho kabla ya kipengele kinachofuata kufundishwa.Hivyo katika upimaji huu mwalimu anaweza kutumia zana zifuatazo:

1.Orodha hakiki ya kupima taaluma
Ni zana mojawapo ya Upimaji inayotumika kupima mabadiliko na mwelekeo wa mwanafunzi kimwelekeo,kiustadi na kiujuzi .
2.Mazoezi
Ni zana nyingine ambayo mwalimu anaweza kutumia kupima maendeleo ya mwanafunzi.mazoezi yanaweza kutolewa kama maswali na maelekezo ya utekelezaji ili kupima kiwango cha uelewa wa mwanafunzi kuhusiana na somo lililofundishwa.vilevile mazoezi yanaweza kutumika kama njia ya kukazia maarifa mapya yaliyofundishwa kwa kila mada.
3.Majaribio
Majaribio hupima kiwango cha ufahamu,uelewa na mabadiliko ya mwenendo na ujuzi/vitendo vya mwanafunzi katika mambo mbalimbali.jaribio linaweza kutolewa kabla ya kufundisha au baada ya kufundisha.Zana hii humwezesha mwanafunzi kuelewa uwezo wake na kumpa ari ya kujibidiisha zaidi katika kujifunza.

UPIMAJI TAMATI
 huu unatumika kujua kama wanafunzi amepata maarifa, stadi na mielekeo katika nyanja zote za kielimu kama ilivyoorodheshwa katika mhtasari wa somo husika.Upimaji wa aina hii hutolewa mwisho wa kipindi cha mafunzo au baada ya mwanafunzi kumaliza ngazi fulani ya elimu.Upimaji huu una lengo la kupima kiwango cha mafanikio kwa ajili ya kuendelea na mafunzo ya juu pamoja na kutunuku mwanafunzi cheti.

UPIMAJI TATUZI
Wanafunzi hutofautiana katika kujifunza.Kuna wanafunzi ambao huelewa haraka na wengine ambao ni wazito kujifunza.Tofauti hizo zinapojitokeza mwalimu ajaribu kufanya Upimaji tatuzi ili kuona mwanafunzi ana matatizo gani katika kujifunza kisha ayatatue.Endapo mwalimu ataona kuwa mwanafunzi anaendelea kuwa mzito katika somo itabidi afanye uchunguzi wa kina ili atatue tatizo Hilo.Lengo la Upimaji wa aina hii ni kutafuta kwa undani sababu zinazomfanya mwanafunzi awe mzito wa kujifunza ili ziwekewe mkakati wa kuziondoa.

NYANJA ZA UPIMAJI WA KIELIMU NA NGAZI ZAKE
Nyanja ni maeneo makuu ya ujuzi,matendo na mwelekeo ambao mwanafunzi anatarajiwa kuwa nayo baada ya mafunzo.Nyanja hizo ni utambuzi, vitendo na mwelekeo/mwenendo

NYANJA ZA UTAMBUZI (COGNITIVE)
Hapa tutajikita zaidi katika kipengele cha utambuzi.
Kipengele cha utambuzi huhusisha:
  • Maarifa
  • Ufahamu
  • Matumizi
  • Uchambuzi
  • Uundaji
  • Tathmini
1.Maarifa
Kinacholengwa katika kipengele hiki ni kujenga taswira ya dhana, tukio au tendo liote mzizi kwenye sehemu inayohifadhi mambo ndani ya ubongo wa mwanandamu. Mwanafunzi anatakiwa aweze kukumbuka kile alichofundishwa na kutaja kwa kauli au maandishi.

2.Ufahamu
Katika kipengele hiki mwanafunzi anatakiwa aweze:
Kutafsiri
Kufupisha
Kubashiri
Kuandika kwa muhtasari
Mifano ya vitenzi vya upimaji ni: fupisha, bashiri, andika muhtasari.
Mfano :- andika namba inayofuata katika mfululizo huu: 2,4,6,8……

3.Matumizi
Hapa kinachosisitizwa ni matumizi ya maarifa hali halisi. Mwenendo unaojengwa hapa ni ule uwezo wa mwanafunzi kutumia ujumbe, kanuni na fikra za maarifa ya ufahamu alionao katika mazingira halisi. Mfano wa vitenzi vya upimaji ni:- tumia, badili sentensi zifuatazo kuwa katika hali fulani, chambua nomino, kitenzi, onesha, kazia, n.k.

4.Uchambuzi
Kipengele hiki kinahusu;
  • Uchambuzi wa dhana
  • Tukio
  • Maarifa fulani
Katika uchambuzi, ufundishaji hulenga kumwezesha mwanafunzi kuchunguza na kutaja uhusiano wa mambo. Mifano ya vitenzi vya upimaji ni:- chambua, husianisha, fafanua, tofautisha, pangua, tenganisha, pambanua, n.k
Advertisement
Mfano: Chambua sentensi ifuatayo: Mtoto anasoma kitabu

5.Uundaji
Katika kipengele hiki, upimaji hulenga uwezo wa mwanafunzi katika kugundua, kuvumbua au kuunda jambo. Mfano: kuandika sentensi kwa namna ya kipekee, kugundua kanuni, kutoa jumuisho, n.k.
Mifano ya vitenzi vya upimaji ni:- Unda, unganisha, panga, weka pamoja, jumuisha, panga maneno yafuatayo ili yalete maana au sentensi kamili. Anapika kitamu mama chakula jikoni.

6.Tathmini
Kipengele hiki ni kama mwamvuli wa vipengele vingine vyote. Kinachoongezeka hapa ni vigezo vinavyowekwa katika upimaji wa uhalaliau ubatili wa jambo; mfano Uzuri wa jambo, n.k. mifano ya vitenzi vya upimaji ni:- tathmini, toa uamuzi, chagua, toa maoni yako, n.k. mfano: Ipi kati ya njia zifuatazo ni sahihi kuhifadhi mazingira? “kupanda miti au kulima kando kando ya vyanzo vya maji”
Mbinu na Zana za Tathmini
Tathmini ya elimu inaweza kutekelezwa kwa kutumia mbinu na zana tofauti kulingana na mahitaji ya wanafunzi ambayo ni:-
1.Kuchunguza kwa makini
2.Mitihani
3.Maswali ya dodoso
4.Mahojiano ya ana kwa ana, n.k.
          NB: Mitihani hutumika zaidi katika tathmini ya elimu

0 Comments:

Advertisement